Monday 15 August 2016

BASATA yamfungulia Nay wa Mitego, yamweka kwenye uangalizi

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungulia Nay wa Mitego kuendelea na shughuli za sanaa baada ya kuwa ametekeleza adhabu (maagizo) zote alizopewa kama masharti ya kumfungulia.
Nay akiwa na Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey L. Mngereza
Chini ni taarifa ya BASATA kwa waandishi wa habari:
BASATA kama mlezi wa wasanii linamfungulia kufuatia yeye mwenyewe (Nay wa Mitego) kujutia na kukiri kwamba amejifunza na yuko tayari kubadilika na kwamba hatarudia makosa aliyoyafanya
Hata hivyo, pamoja na kumfungulia kuendelea na shughuli za Sanaa Baraza linamweka kwenye uangalizi maalum msanii huyo kama sehemu ya kuhakikisha anaendesha shughuli za Sanaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu sambamba na kuzingatia maadili katika kazi zake.
Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 27/07/2016 Baraza lilimfungia Msanii Nay wa Mitego kwa kipindi kisichojulikana na kumtaka kutekeleza maagizo yafuatayo:
1. Kuhakikisha amesajiliwa na kuwa na kibali cha kuendesha shughuli za Sanaa
2. Kulipa faini ya shilingi milioni moja (1,000,000/-)
3. Kuomba radhi watanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari na kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii
4. Kuufanyia marekebisho wimbo wa ‘Pale Kati’ ili ubebe maudhui yenye maadili
Msanii Nay wa Mitego ametekeleza adhabu zote tajwa hapo juu. Leo hii tunamkabidhi rasmi cheti chake cha usajili na kibali cha BASATA.
Hata hivyo, pamoja na kuleta marekebisho mara mbili ya wimbo wa ‘Pale Kati’ Baraza bado halijaridhishwa na marekebisho hayo hivyo linaendelea kuufungia wimbo huu hadi hapo litakapojiridhisha umekidhi vigezo vya kimaadili.
Katika kikao na Msanii Nay wa Mitego cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa adhabu yake kilichofanyika tarehe 12/08/2016 Ofisi za BASATA ameagizwa kuendelea kuufanyia marekebisho wimbo wake huo kama bado anaona anauhitaji.
Baraza linatoa maelekezo kwa vyombo vya habari na watanzania kwa ujumla kuacha kuucheza wimbo huo hadi hapo itakapoelekezwa vinginevyo. Hatua na adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa chombo chochote cha habari kitakachokiuka agizo hili.
Aidha, katika kikao hicho cha tathimini ilibainika kwamba Msanii Nay wa Mitego kwa taarifa potofu alizopewa alipanda Jukwaani kwenye tamasha la Mwendo Kasi la tarehe 30/07/2016 akiwa katika adhabu. Kwa kosa hili ameandika barua ya kuomba radhi na Baraza linafikiria hatua za kuchukua kwa waandaaji wa tamasha hilo.
Baraza linatoa wito kwa wasanii kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za Sanaa sambamba na kuhakikisha wanazingatia maadili katika kila kazi wanazobuni ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima ambayo yanaathiri kazi zao kwa kiasi kikubwa sana

Related Posts

BASATA yamfungulia Nay wa Mitego, yamweka kwenye uangalizi
4/ 5
Oleh

Subscribe via email

Like the post above? Please subscribe to the latest posts directly via email.