Friday 17 November 2017

MSIBA WA NDIKUMANA WAMTESA UWOYA


Staa wa Bongo, Irene Pancras Uwoya.
WAKATI kifo cha aliyekuwa mume wa staa wa sinema za Kibongo, Irene Pancras Uwoya, Hamad Ndikumana Katauti (39), raia wa Rwanda kilichotokea usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii, kikiibua utata kutokana na mshtuko wake, hali hiyo kwa mkewe huyo inafananishwa na kile kilichomkuta mwanamama Zarinah Hassan Tiale ‘Zari The Boss Lady’ kwa mumewe, Ivan Ssemwanga ‘Don Ivan’ miezi kadhaa iliyopita.
VYANZO VYA RWANDA
Kwa mujibu wa vyanzo kutoka nchini Rwanda, chanzo cha kifo cha mume wa Uwoya ni matatizo ya moyo huku kikishangaza kwani jana yake (Jumanne) alikuwa fiti akiendelea na kazi zake kama kawaida.
Hadi anakutwa na umauti, Ndikumana alikuwa Kocha Msaidizi wa Timu ya Rayon Sports ya Rwanda ambapo saa kadhaa kabla ya umauti alikuwa akifanya mazoezi na wachezaji wake.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Afisa Habari wa Rayon Sports, Gakwaya Olivier alisema kuwa, Ndikumana alifariki kwa kile kilichosadikiwa kuwa ni ugonjwa wa moyo.
UTATA
Utata wa kifo cha Ndikumana unaelezwa kutokana na namna kifo hicho kilivyotokea ghafla.
“Alisikia maumivu makali kifuani, akaomba soda ya baridi, wakamletea na alipomaliza kunywa kidogo tu, alitapika kisha akaishiwa pumzi na ndipo akakata kauli,” alisema afisa habari huyo.
Akiwa katika pozi.
NDOA YA UWOYA NA DOGO JANJA YATAJWA
Wakati simanzi hiyo ikizua mjadala mkali, baadhi ya watu walidai kuwa, matatizo hayo ya moyo huenda yalitokana na msongo kufuatia mkewe huyo ambaye alikuwa hajampa talaka kudaiwa kufunga ndoa na msanii wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ hivi karibuni.
Wachambuzi wa matukio ya mastaa Bongo walieleza kuwa, baada ya stori za Uwoya na Dogo Janja kuibua mjadala mzito, Ndikumana alikuwa akiposti maneno ya mafumbo mitandaoni kabla ya kumtambulisha mpenzi wake mpya.
UWOYA YAMKUTA YA ZARI
Ilisemekana kwamba, kifo cha mume huyo wa Uwoya kinatengeneza mazingira kama yale ya kifo cha mume wa Zari, Ivan ambaye naye alikutwa na umauti kutokana na matatizo ya moyo na baadaye kufuatiwa na mama yake.
NDIKUMANA KAMA IVAN
“Kifo cha Ivan na chenyewe ilidaiwa kilitokana na msongo baada ya Zari kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine kama ilivyo kwa Ndikumana baada ya Uwoya kudaiwa kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Dogo Janja,”
kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Kilichomkuta Uwoya kinafanana kabisa na kile kilichotokea kwa Zari kwani utagundua kuwa wote waliingia kwenye mapenzi na wasanii wa Bongo Fleva.
Irene Pancras Uwoya na Hamad Ndikumana Katauti (39) enzi wakiwa pamoja.
HAKUKUWA NA TALAKA
“Kama hiyo haitoshi, wote walikuwa hawajapewa talaka na waume zao na hata ugonjwa uliowasababishia waume zao umauti ni ugonjwa wa moyo.
“Pia wote vifo vyao vilikuwa vya ghafla kwani hawakuripotiwa kuwa wanaumwa.
BADO WALIWAHITAJI
“Kibaya zaidi wote walisharipotiwa kuwa wapo kwenye hali mbaya kutokana na kutoswa na wake zao ilihali wakiwa bado wanawahitaji.
“Ivan alikuwa akimbembeleza Zari kumrudia kama ilivyokuwa kwa Ndikumana ambaye miezi
kadhaa iliyopita alikaririwa akisema kuwa, amekuwa akimuomba Uwoya arudi kwake waendelee na maisha hasa katika suala la kumlea mtoto wao wa kiume aitwaye Krish.
Kwa upande wake, Ivan alikutwa na umauti Mei 30, mwaka huu ambapo katika ndoa yake na Zari, walijaliwa watoto watatu wa kiume, Pinto, Didy na Quincy.
MAMA UWOYA AANIKA SIRI
Kwa upande wake mama Uwoya, Naima Uwoya alianika siri ya kushangaza juu ya mwanaye huyo na Ndikumana ambapo alisema kuwa, alihangaika mno kurudisha uhusiano wa wawili hao lakini ikashindikana.
Mama Uwoya alisema kuwa, katika kurejesha ndoa hiyo, alikwenda hadi nchini Israeli kwa ajili ya kufunga na kumuomba Mungu ili wawili hao wamalize tofauti zao na aliamini ipo siku mambo yangekuwa sawa, lakini ndiyo hivyo Mungu naye alikuwa na mipango yake.
MAZISHI YA NDIKUMANA YATIKISA
Ndikumana alizikwa Jumatano iliyopita nchini Rwanda ambapo mazishi yake yalitikisa kutokana na uwepo wa ndugu na marafiki wengi waliojitokeza katika mazishi hayo.
Uwoya alishindwa kwenda kumzika kwa kile kilichoelezwa na watu wake wa karibu kuwa alikuwa jijini Dar na ilikuwa ni ghafla mno hivyo leo (Ijumaa) anatarajiwa kwenda kuhani msiba nyumbani kwa Ndikumana jijini Kigali, Rwanda akiongozana na wasanii wenzake wa Bongo Muvi.
TIMU ALIZOCHEZEA NDIKUMANA
Hadi anakutwa na umauti, Ndikumana aliyezaliwa Oktoba 5, 1978, aliwahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo Rayon Sports na Timu ya Taifa ya Rwanda kuanzia mwaka 1998 na kuwa nahodha wa muda mrefu wa timu hiyo iitwayo Amavubi.
Pia alicheza soka la kulipwa Ulaya katika Timu za Gent na Anderlecht za Ubelgiji, Omonia Nicosia na Limassol za nchini Cyprus kabla ya kumalizia soka lake la uwanjani akiwa na Stand United ‘Chama la Wana’ ya nchini Tanzania.
TULIKOTOKA
Julai 11, 2009, Ndikumana alifunga ndoa na Uwoya katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar kabla ya ndoa yao kuvunjika rasmi miaka minne iliyopita.

Source: global publishers

Related Posts

MSIBA WA NDIKUMANA WAMTESA UWOYA
4/ 5
Oleh

Subscribe via email

Like the post above? Please subscribe to the latest posts directly via email.